"Adui amevuka mistari yote myekundu na sheria zote katika shambulio hili. Hili ni shambulio kubwa la kigaidi na ni mauaji ya halaiki, " Sayyid Hassan Nasrallah alisema Alhamisi katika hotuba yake ya kwanza ya televisheni tangu shambulio hilo.
"Mauaji ya Jumanne na Jumatano ni uhalifu wa kivita, tangazo la vita...unaweza kuiita chochote," alisema, akiongeza Israel itakabiliwa na "adhabu kali na ya haki ya kulipiza kisasi, pale inapotarajia na pale isipotarajia".
Nia ya Israel, Nasrallah alisema, ilikuwa kuua watu 4,000 wa Lebanon ndani ya dakika lakini wakati wa hujuma hiyo idadi kubwa ya pager zilikuwa hazitumiki.
"Wakati adui walipopanga kufanya shambulizi hili, walidhani kwamba kulikuwa na angalau pager 4,000 zilizoenea katika Lebanon yote. Hii ina maana kwamba adui alikuwa na nia ya kuua watu 4,000 kwa dakika moja.
"Hayo yalirudiwa siku ya pili kwa lengo la kuua maelfu ya watu waliokuwa wamebeba vifaa vya redio," Nasrallah alisema.
Baadhi ya mashambulizi hayo, alisema, yalifanyika katika hospitali, maduka ya dawa, sokoni, maduka ya biashara na hata makazi ya watu, magari ya kibinafsi na barabara za umma ambako maelfu ya raia, wakiwemo wanawake na watoto, wapo.
Nasrallah alisema kamati ya kina ya uchunguzi imeundwa kuchunguza matukio yote, uwezekano, na nadharia, na hitimisho la karibu kufikiwa.
Siku ya Jumanne, Walebanon wasiopungua 14 waliuawa shahidi na wengine zaidi ya 3,000 walijeruhiwa kutokana na miripuko ya vifaa vya mawasiliano visivyotumia waya (pager) katika maeneo tofauti ya Lebanon, ambapo miripuko hiyo ilitekelezwa na utawala wa Kizayuni.
Nasrullah ametoa mkono wa pole kwa familia za mashahidi waliofariki dunia Jumanne na Jumatano, kufuatia mauaji ya Israel ya idadi kubwa ya raia wa Lebanon, kwa kuripua vifaa vya mawasiliano (pager); na kuwatakia afueni ya haraka wale waliojeruhiwa katika tukio hilo.
Sayyid Nasrallah amepongeza Umoja wa Kitaifa wa Walebanon katika kukabiliana na chokochoko hizo mpya za Israel. "Moja ya baraka za damu hii tukufu ni taswira ya kipekee ya ubinadamu tuliyoshuhudia kote Lebanon," alibainisha.
Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesema adui Mzayuni alitumia zana ya kiraia inayotumiwa na makundi makubwa ya jamii, na akafanya hivyo tena siku ya Jumatano kwa kuripua vifaa visivyotumia waya.
Nchi mbali mbali duniani zimelaani vikali operesheni ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Harakati ya Hizbullah iliyopelekea kuuawa shahidi watu kadhaa na kujeruhiwa idadi kubwa ya raia wa Lebanon.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Sayyid Nasrallah aliwapongeza Waislamu kwa kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) na Wiki ya Umoja wa Kiislamu.
3489968